TAMKO LA RAISI KIKWETE JUU YA MLIPUKO WA BOMU ULIOTOKEA OLASITI ARUSHA
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya tukio la leo,
Jumapili, Mei 5, 2013 la mlipuko kwenye Kanisa Katoliki la Mt. Joseph
Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha.
Tukio
hilo la kigaidi limesababisha mtu mmoja kupoteza maisha na wengine 40
kujeruhiwa. Rais Kikwete analaani vikali shambulio hilo lililofanywa na
mtu au watu katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa
Tanzania na watu wake.
Rais
Kikwete ameagiza vyombo vya usalama nchini kumsaka mtu au watu
waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha kwenye vyombo vya
sheria. Vile vile Rais Kikwete amewataka wananchi wote kuwa watulivu
wakati Serikali na vyombo vyake inaendelea kufuatilia tukio hili.
Tutawasaka
popote walipo na kupambana nao bila huruma. Aidha, tutakabiliana na
aina yoyote ya uhalifu nchini iwe ni ugaidi au aina yoyote ya uhalifu wa
namna hiyo au wa namna nyingine, uwe na chimbuko lake ndani ya nchi ama
nje ya nchi yetu.
Kamwe
hatutakubali kuwaacha wavuruge amani na usalama wa Tanzania na watu
wake. Rais anaamini kuwa Serikali, kwa msaada na ushirikiano wa
wananchi, watu hao watapatikana na kuadabishwa ipasavyo.
Aidha,
Rais Kikwete anatoa rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wafiwa na wale
wote ambao wamejeruhiwa katika tukio hilo. Anaungana nao katika machungu
na msiba. Rais pia anawaombea wote walioumia katika tukio hili wapate
nafuu ya haraka na waendelee na shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Rais
Kikwete vilevile anatoa pole nyingi kwa viongozi na waumini wa Kanisa
Katoliki kwa tukio hili la kusikitisha na kuvurugika kwa ibada na
shughuli yao muhimu ya uzinduzi wa Kanisa lao.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
5 Mei, 2013
Post a Comment