Header Ads

test

WATUHUMIWA WA MLIPUKO WA BOMU OLASITI WAACHIWA HURU

POLISI Jijini Arusha imewaachia kwa dhamana watu wanaotuhumiwa kurusha bomu kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, lililopo Jijini hapa. Aidha Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema, wanaendelea kuwahoji zaidi watu hao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda Sabas amesema, wameamua kuwaachia kwa sababu sheria haiwaruhusu kuendelea kuwashikilia muda mrefu.
“Na lengo letu hasa katika hili tukio hatutaki kumwonea mtu yeyote, ndio sababu tunafanya uchunguzi wa kina,” alisema Sabas.
Alisema watuhumiwa hao ni lazima waripoti polisi, pale wanapohitajika. Alisema hadi sasa hakuna mtu mwingine aliyekamatwa au kufikishwa mahakamani zaidi ya Victor Ambros aliyefikishwa mahakamani.
Ambros alifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya kuua na kukusudia kuua huku wengine wanne, raia wa nje ya nchi wakiachiwa huru.
Awali watuhumiwa waliokuwa wakiendelea kushikiliwa kwa uchunguzi zaidi ni Jassini Mbarak (29) mkazi wa Bondeni Arusha, Joseph Lomayani (18) dereva wa pikipiki mkazi wa Kwa Mrombo Arusha, Batholomeo Silayo (23) mfanyabiashara mkazi wa Olasiti na Mohamed Suleiman Said (38) mkazi wa Ilala Jijini Dar es Salaam.
Raia wa Falme za Kiarabu ambao wote walioachiwa huru, ni Abdulaziz Mubarak (30) (Saudi Arabia), Foud Saleem Ahmed (28), Said Mohsen na Said Abdallah Said (28).
Wote wanaishi nchini humo. Bomu hilo lililorushwa Mei 5, mwaka huu, saa 4.30 asubuhi, lilisababisha vifo vya watu watatu na majeruhi wapatao 60.
Majeruhi hao walipatiwa matibabu katika Hospitali za Mount Meru na St. Elizabeth na baadhi yao walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Katika ibada hiyo ya uzinduzi wa Parokia mpya ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, mgeni rasmi alikuwa Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisco Padilla, akisaidiana na Askofu wa Jimbo Kuu la Arusha, Joseph Lebulu.

source by HABARILEO