Sheikh Issa Ponda:Serikali inataka kufuta masomo ya dini
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Nchini, Sheikh Issa Ponda, ameitaka Serikali itoe tamko mara moja kuhusu kufuta mitalaa ya masomo ya dini.
Amesema kitendo hicho ni cha kuwanyima haki Watanzania kupata elimu ya dini.
Pia, amesema wao kama wawakilishi wa Waislamu
watahakikisha kuwa wanatetea haki ya wanafunzi kupata elimu hiyo, ili
kusaidia taifa kuwa na watu wenye maadili.
Akizungumza katika mkutano wa Waislamu kutoka
mikoa mbalimbali nchini, alisema wanatambua mipango ya Serikali ya
kutaka masomo hayo yasifundishwe ili kuwakandamiza Waislamu.
“Tumegundua mbinu mbalimbali zinazofanywa na
Baraza la Mitihani la Taaifa (Necta) na Serikali ili kuhakikisha kuwa
masomo ya dini yanafutwa. Jumuiya ya Kiisalamu Nchini tunaitaka Serikali
itoe tamko la kuruhusu masomo hayo yaendelee kufundishwa haraka
iwezekanavyo kuanzia sasa,” alisema Sheikh Ponda.
“Hata hivyo tunataka ifahamike kwamba Waislamu
hatujashirikishwa kwenye vikao vyovyote vya kujadili mapendekezo kuhusu
masomo hayo kama walivyo shirikisha wenzetu wa upande wa pili,”
alisisitiza
Alisema kilichotokea katika kikao ambacho wao
wanakifahamu, walipeleka makubaliano waliyofikia ikiwa ni pamoja na
kufuta mitalaa hiyo kwenye Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata)
bila hata baraza hilo kushirikishwa.
Mwenyekiti wa Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislamu
Nchini, Hussein Pilly, alisema mbinu za Serikali ni kutaka kuyaondoka
kabisa masomo ya dini shuleni kitu ambacho hakiwezi kukubalika.
“Leo Serikali inafuta mitaala ya masomo ya dini,
hatujui nia yao ni kitu gani, sasa sisi tunasema kwamba hatuungi mkono
jambo hilo na tunalipinga kwa nguvu zote,” alisema.
Alisema kufanya hivyo ni kuwanyima haki ya msingi Watanzania wanaohitaji kupata elimu hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Selestine Gesimba, ilisema Serikali
haijafuta Mitihani ya Taifa ya masomo ya Dini kama inavyodaiwa na baadhi
ya watu.
“Masomo ya dini yanaendelea kufundishwa shuleni na
kutahiniwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) hakuna somo
lililofutwa au kuondolewa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.” ilisema
sehemu ya taarifa hiyo.
www.mwananchi.co.tz
www.mwananchi.co.tz
Post a Comment