Header Ads

test

UTALII WA NDANI:Haya Ndiyo Magari Yaliyotumiwa Na Hayati Baba Wa Taifa Mwalimu Nyerere

Leo tupo katika utalii wa ndani kwa kutazama baadhi ya  magari aliyotumia Baba wa Taifa na Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa harakati za Uhuru na baada ya Uhuru mpaka alipofariki Oktoba 14,1999. Maelezo ya makala haya ni kwa mujibu wa nyaraka zilizopo Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam hasa kuhusiana na magari na miaka ya magari yalipotumika. Fuatana nasi.
1.AUSTIN MORRIS A-40

AUSTIN MORRIS A-40
 Gari aina ya  Austin Morris A-40 lilitengenezwa nchini Uingereza kati ya mwaka 1940 – 1950. Ni gari la kwanza kutumiwa na Baba wa Taifa na Rais wa kwanza Tanzania hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mwalimu Nyerere alilitumia gari hilo toka mwaka 1955 – 1960 katika shughuli mbalimbali za kuendeleza chama cha TANU likiendeshwa na dereva wake maarufu kwa jina la SAID TANU. Baadaye Mwalimu Nyerere alilikabidhi gari hilo kwa vijana wa TANU kwa kazi za chama kabla ya kupelekwa Makumbusho ya taifa na kuwa sehemu ya Historia ya Tanzania.
2. AUSTIN MORRIS (A-40 VAN GUARDS)
AUSTIN MORRIS (A-40 VAN GUARDS)
Gari aina ya Austin Morris A-40 maarufu kama Van Guards lilitengenezwa kati ya miaka ya 1945 – 1950. Gari hili lilitumiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa shughuli za TANU akiwa Dar es Salaam na ziara za mikoani kuhamasisha shughuli za chama. Dereva wake alikuwa ni SAID TANU.
3.ROLLS ROYCE
ROLLS ROYCE
 Gari aina ya ROLLS ROYCE lilitengenezwa  1938 na kuletwa na Gavana wa wakati huo Harold Mac Michael katika utawala wa wakoloni waingereza na lilitumiwa na Gavana wa mwisho kuitawala Tanganyika Sir Richard Turnbull.
Rolls Royce lilitumika kupokea wageni mbalimbali waliotembelea Tanganyika wakati huo wakimwemo Rais wa zamani wa Liberia Hayati William Tubmann na Mfalme wa zamani wa Ethiopia Hayati Haille Sellasie.
Gari hilo lilitumika hadi mwaka 1962 baadaye  mwaka 1978 Rais wa kwanza Tanzania Hayati Julius Kambarage Nyerere aliagiza Rolls Royce kuhamishwa toka Ikulu hadi Makumbusho ya Taifa. Kwa sasa ni sehemu ya Historia ya Taifa la Tanzania.
4. ROLLS ROYCE (PHANTOM V)
ROLLS ROYCE (PHANTOM V)
 Gari aina ya Rolls Royce Phantom V lilitengenezwa nchini Uingereza na kutolewa na nchi hiyo kwa Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Novemba 05,1965.
Rolls Royce  Phantom V lilianza kutumika mwaka 1970 kwa kupokea viongozi wa nchi mbalimbali wakiwemo Marais na mabalozi wa nchi mbalimbali waliotembelea Tanzania.
Gari hilo lina sifa za kipekee kwa wakati huo likionekana la  kisasa zaidi kwani lina sehemu ya mbili za kuweka bendera, moja upande wa kulia ambako aliketi mgeni na upande wa kushoto bendera ya Tanzania alikoketi mwenyeji wake (Mtanzania). Sehemu ya juu ya  Rolls Royce Phantom V yaweza kufunguliwa kwa minajili ya kuwaruhusu viongozi kusimama na kuwapungia mikono wananchi au kuruhusu hewa kuingia hasa wakati wa joto (hapa ni kama AC/kiyoyozi kwa magari ya sasa). Kwa kweli tumetoka mbali na huu ndio uhondo wa historia.
 
Rais wa awamu ya pili wa Tanzania Alhaji Ali Hassan Mwinyi alilitumia gari hilo na Rais wa awamu ya tatu Benjamini William Mkapa akalitumia pia kabla ya kuamua kulipeleka Makumbusho ya Taifa Machi 08,2006 na kuwa sehemu ya Historia ya Tanzania.
5.MERCEDEZ BENZ 230.6
Mercedez Benz 230.6 lilijulikana kama gari la jumuiya kwani lilitumiwa na Rais wa Tanzania Hayati  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa shughuli za jumuiya Afrika Mashariki iliyoundwa mwaka 1967 na nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ambapo kila nchi ilikuwa na gari kama hilo.
Moja ya sifa ya gari hilo kwa wakati huo ni kuwa na uwezo wa kubeba watu wengi zaidi.Uwezo wake ni kubeba marais wageni wawili, mpambe wa Rais, mwandishi habari wa Rais na Rais mwenyeji kwa mara moja.
Mercedez Benz 230.6 lilikuwa na namba za kipekee ambazo ni RE-1 (yaani Royal Excellecy 1).Hata hivyo Jumuiya ya kwanza ya Afrika Mashariki ilidumu kwa miaka 10 tu (1967 – 1977) ambapo ilivunjika kwa sababu mbalimbali. Gari  hilo likapelekwa Makumbusho ya Taifa Oktoba mwaka 2002 na kuwa sehemu ya Historia ya Tanzania.
MERCEDEZ BENZ E 300

MERCEDEZ BENZ E 300
 Mercedez Benz E 300 lilitengenezwa nchini Ujerumani na kununuliwa na serikali ya Tanzania Desemba 17, 1996  ambapo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alilitumia kwa shughuli za kitaifa na binafsi katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani baada ya kustaafu Urais.
Mercedez Benz E-300 litaendelea kukumbukwa zaidi kwani ndilo gari la mwisho kwa Hayati Mwalimu Nyerere kulitumia enzi za uhai wake hapa nchini kwani alilitumia kwa mara ya mwisho kabisa Agosti 31,1999 akienda kupata matibabu huko nchini Uingereza.
Alisafiria gari hilo kutoka nyumbani kwake Msasani hadi uwanja wa kimataifa wa Dar es Salaam (kwa sasa Mwalimu Julius Nyerere).
Hata hivyo kwa MASIKITIKO MAKUBWA Baba wa Taifa hakurudi tena kulitumia tena gari hilo kwani alifariki dunia Oktoba 14, mwaka 1999 katika hospitali ya Mtakatifu Thomas huko nchini Uingereza. MUNGU AIWEKE ROHO YAKE MAHALA PEMA PEPONI,AMEN.
Gari lake alilotumia kwa mara ya mwisho (Mercedez Benz E 300) likatolewa na mkewe Mama Maria Nyerere kwa ajili ya kuhifadhiwa katika Makumbusho ya Taifa Septemba 24, 2004.
Katika utalii wa ndani tumeangazia kipengele kidogo tu cha usafiri kwa kuangalia magari aliyotumia Rais wa kwanza Tanzania Hayati  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wenzake hivyo kama Watanzania nadhani kuna mambo mengi ya kujifunza kupitia utalii wa ndani hasa wa Kiutamaduni na kuangalia historia mila na desturi za Watanzania kabla na wakati wa ukoloni hatimaye baada ya Uhuru. 
Kuna mambo mengi ambayo Watalii kutoka nchi za nje wanayafahamu kuliko Watanzania wenyewe. Mathalani, mtu wa Bagamoyo hajui historia ya mji wa kale ya Kaole, Caravan Serai na mengineyo huku mtu wa Dar es Salaam akishindwa kufika Makumbusho ya Taifa jijini humo au kijiji cha Makumbusho Kijitonyama kujua Historia mbalimbali. Vivyo hivyo, Mtanzania anayeishi Mikumi, Kilimanjaro au Serengeti anashindwa kujua mambo yanayomzunguka huku mtu kutoka Ujerumani au Marekani anafahamu mengi kuhusu maeneo. Hii ni changamoto kubwa kwa Watanzania.
Kuna watu wanasema umasikini wa kipato lakini wale wanaozunguka maeneo hayo mara nyingi viingilio ni bei ambayo Mtanzania anaweza kumudu mathalani shilingi elfu miatano (1500) kuingia katika Makumbusho ya Taifa, ukitoka Magomeni jijini utatumia nauli shilingi 600 kwenda na kurudi maeneo ya Posta. Ni ukweli usiopingika kuwa uchumi umeyumba kwa wananchi lakini mwananchi huyo huyo ana uwezo wa kununua bia 3 – 5 kila siku lakini hana uwezo wa kugharamia shilingi elfu 1500 au 5000 kwa kutembelea kivutio kimojawapo karibu na anapoishi angalau mara moja kwa mwaka. ….huenda kuna lingine zaidi ya kipato.
Afisa Elimu wa Makumbusho ya Taifa Mawazo Ramadhani anasema mwamko wa watanzania ni mdogo hasa utalii wa kiutamaduni huku akikiri kupokea makundi makubwa ya wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo na wageni kutoka nje.
Utalii wa kiutamaduni unahusisha vitu ambavyo mwanadamu anavizalisha kila siku mavazi,mila na desturi za jamii ya watanzania.
Hata hivyo Afisa elimu huyo amesema katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakipokea watalii wa ndani hasa familia katika siku za wikiendi na sikukuu jambo linalotia faraja kwa kiasi kikubwa katika sekta hiyo.Kila laheri kuelekea maadhimisho ya mwaka mpya 2013.
 
source songafesto blog