Header Ads

test

BHAKRESSA NDO TAJIRI WA BONGO LAND

Swali kwamba ni nani anaongoza kwa utajiri hapa nchini Tanzania tayari limepatiwa majibu na ukweli wa kitafiti unathibitisha kuwa mfanyabiashara mwenye njaa ya kujitanua kila kukicha, Said Salim Bakhressa ndiye tajiri nambari moja Bongo.
Utafiti huo, unathibitisha kuwa Bakhressa yupo mbele ya wafanyabiashara wakubwa nchini, Reginald Mengi, Yusuf Manji, Mustafa Sabodo, Mohammed Dewji, Rostam Azziz, Tanil Somaiya,  Jeetu Patel, Subhash Patel na wengineo.

Jarida la Marekani, Forbes ambalo limepata umaarufu na heshima kubwa kwa tafiti mbalimbali na utoaji wa ripoti za utajiri na matajiri ulimwenguni, limemtaja Bakhressa miongoni mwa watu 40 wanaoongoza kwa utajiri barani Afrika.
Katika ripoti mpya, ikiwa na utafiti uliofanywa mpaka Novemba 2012, Forbes limemtaja Bakhresa kuwa anashika nafasi ya 30 katika matajiri 40 wa Afrika.
Ripoti hiyo, inaonesha kwamba Bakhressa anashika nafasi ya pili kwa utajiri Afrika Mashariki, akiwa nyuma ya ‘tycoon’ wa Uganda, Sudhir Ruparelia ambaye anamiliki utajiri unaotajwa kufikia dola za Marekani milioni 900 (zaidi ya shilingi trilioni 1.4).
Bakhressa yeye ametajwa kwamba anamiliki utajiri unaofikia dola za Marekani milioni 520 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 832.
TAJIRI NAMBA MOJA AFRIKA
Tajiri nambari moja Afrika ametajwa kuwa ni raia wa Nigeria, Aliko Dangote ambaye utajiri wake una thamani ya dola bilioni 12 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 19.2.
Asili ya utajiri wa Dangote ni biashara ya peremende lakini sasa hivi amekuwa mwekezaji wa kutisha akimiliki viwanda vya saruji, sukari, unga na bidhaa mbalimbali.
MWANAMKE TAJIRI AFRIKA
Folorunsho Alakija mwenye umri wa miaka 61 ndiye tajiri nambari moja kwa wanawake, huku katika orodha ya jumla katika matajiri 40 wa Afrika, akikamata nafasi ya 24.
Folorunsho, raia wa Nigeria, ana utajiri wa dola za Marekani milioni 600 sawa na shilingi bilioni 960, wakati mwanamke anayeshika nafasi ya pili ni Isabel dos Santos, 39, wa Angola anayemiliki utajiri wenye thamani ya dola za Marekani milioni 500 ambazo ni sawa ni shilingi bilioni 800.
Kawa jumla katika orodha ya matajiri 40 Afrika, wanawake waliong’ara ni wawili tu, yaani Folorunsho na Isabel.
AFRIKA KUSINI, NIGERIA ZAFUNIKA
Katika orodha ya matajiri 40, Afrika Kusini ndiyo iliyoongoza kwa kuingiza matajiri 13, wakati Nigeria imeshika nafasi ya pili ikiwa na watu 11, Misri ni ya tatu ikiingiza nane, Morocco inakamata nambari nne na matajiri wake watano.
Utajiri wa kiukoo ndiyo umeibeba Misri, kwani matajiri saba wanatoka kwenye koo mbili kubwa katika taifa hilo.
Ukoo wa Swarisi umeongoza, baada ya kuingiza watu wanne, wakati ukoo wa Mansour wenyewe umetumbukiza watatu kwenye orodha hiyo ya matajiri 40 wa Afrika.
KUHUSU BAKHRESSA
Said Salim Awadh Bakhresa, alizaliwa mwaka 1949, sasa hivi ana umri wa miaka 63. Historia inaonesha kwamba akiwa na umri wa miaka 14, aliacha shule na kuingia kwenye biashara ya kuuza viazi na baadaye alianzisha mgahawa mdogo.
Hivi sasa, Bakhressa ni mwenyekiti wa Makampuni ya Bakhressa (Bakhressa Group of Companies). Nembo yake ya Azam, imeweza kumpatia umaarufu mkubwa.
Anamiliki viwanda vya vinywaji baridi, biskuti, ice cream, pipi, vilevile ni msambazaji wa bidhaa za chakula Tanzania na sehemu kubwa ya Bara la Afrika kama vile unga, sukari na kadhalika.
Bakhressa pia anamiliki utitiri wa magari ya mizigo, anayo pia mabehewa ya mizigo yenye nembo za Azam katika reli za Kati na Tazara.
Anayo kampuni ya usafirishaji Bahari ya Hindi na Ziwa Victoria inayoitwa Azam Marine ambayo inamiliki maboti na meli nyingi zaidi pia ndiyo inayoongoza kwa kusafirisha abiria kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Kwa upande mwingine, imeelezwa kuwa hata utajiri aliotajwa na Forbes kwamba anaumiliki, inawezekana amepunjwa kwa sababu mwaka 2011 peke yake, inakadiriwa kuwa aliuza bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 800 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 1.2.
BY DEIWAKA