Header Ads

test

Alichokiandika ridhiwan kikwete facebook kuhusu account yake kuhackiwa

Ndugu zangu, habari za mapumziko
ya mwisho wa wiki. Yapo mambo
machache ningependa
kuwashirikisha ili kuweka
kumbukumbu sawa, na pia kuzuia
upotoshaji ambao unaweza
kujitokeza siku za usoni iwe kwangu,
kwako au kwa mtu mwingine.
Mojawapo ya mambo makubwa
ambayo yamejitokeza siku za
karibuni hasa katika suala la
Teknolojia na habari ni jambo la
sheria za faragha (privacy and
privacy laws). Tumeshuhudia
kufungwa kwa gazeti za News of The
World mali ya bilionea Rupert
Murdoch wa Kimarekani baada ya
kudhihirika alitumia wataalam wa
teknolojia (hackers) kutafuta siri za
watu mashuhuri kwa kuingia katika
simu zao za mkononi kinyume cha
utaratibu na sheria za faragha
(Privacy Laws). Tumeshuhudia pia
wahalifu hao hao wa mtandao
wakifanya mengi kama kuvamia kwa
mitandao ya makampuni makubwa
kama Sony na mengineyo na hata
katika mitandao hii ya kijamii upo
wakati marafiki zako wanakwambia
mbona umenitumia kitu
kisichoeleweka, na baadaye kuja
kugundua kwamba si wewe
uliyefanya hivyo.
Tarehe 1, 8 na 9 mwezi huu wa
Machi nilikuwa Dar es Salaam kwa
shughuli zangu za kawaida kimaisha
lakini ziko updates 5 zilifanyika hapa
moja ikimhusu ndugu Absalom
Kibanda. Ni ajabu kwamba baadhi ya
waandishi tena waliojivika taji la
usahihi katika uandishi waliiandika
habari hiyo bila hata kuniuliza
kwamba ni nini kinatokea.
Tunajitahitahidi na kutamani kuwa
na Taifa la waandishi makini na
wenye kufuata maadili lakini wapo
wanaoturudisha nyuma. Ni ajabu
gazeti kuandika jambo lisilo la kweli
huku wahusika wakiwa na kila uwezo
wa kumfikia yule wanayedhani
kwamba ameandika na kumhoji ili
kuhakiki habari. Kazi ya uhariri ni
kuhakiki. Ikiwa mtu atakimbilia
kuandika jambo likuhusulo ambalo
hana hakika nalo na alikuwa na kila
uwezo wa kuwasiliana na wewe na
kukuuliza lazima utajiuliza maswali
mengi. Kwanza, nini hasa lengo lake?
Pili, ufahamu wake wa kile
anachokifanya kwa maana ya
taaluma yake katika kazi
anayoifanya.
Napenda kuwaambia kwamba katika
tarehe hizo mwezi huu wa Machi,
wahalifu wa mtandao wakiwa eneo
la Njiro na baadaye Kijenge mjini
Arusha, kila post ilionyesha eneo
ilipotoka, (wakati huo mimi nikiwa
Dar es Salaam) waliingia bila idhini
kwa njia haramu (Hacking) katika
anuani yangu ya Facebook na ku-
post habari hizo tano. Sasa
nimeliacha jambo hilo katika
vyombo stahiki vya ulinzi na
usalama ili kufuatiliwa kadiri ya
taratibu zao.
Natoa wito kwa ndugu zangu
waandishi kujitahidi kuhakiki habari
kabla ya kuzipeleka katika vyombo
vyao na pia wahariri kuzingatia
kuhakiki habari kabla ya
kuzichapisha hasa kama chombo
chako cha habari si cha habari za
udaku. Hii itasaidia wao kujenga
heshima mbele ya jamii, kufikisha
kile hasa ambacho ni habari na
kuzuia mikanganganyiko isiyo ya
lazima. Haya yakizingatiwa nadhani
hata sintofahamu hizi za uandishi wa
habari unaotokana na hisia na
vyanzo vumbi na ufahamu mdogo
wa jambo utaondoka na tutakuwa na
jamii ambayo haki na uwajibikikaji
wa wanahabari kwa jamii
utaonekana kutendeka.
Niombe radhi kwa ndugu yangu,
rafiki yangu na pia mwalimu wangu,
Ndugu Absalom Kibanda kwa
usumbufu wowote uliojitokeza
ambao naamini watu wasio na nia
njema walitaka kuutumia kuleta
hisia tofauti katika jamii na pia
kumpa pole kwa mara nyingine tena
kwa maumivu yaliyosababishwa na
ujangili huo. Namuombea kwa
Mungu ampe unafuu mapema zaidi
ili arudi katika meza yake
kuendeleze harakati za kupambana
na mchango wake katika kuleta
maendeleo ya kweli kwa nchi yetu.
Nawapa pole pia wale wote ambao
kwa namna moja au nyingine
walikwazwa na uzushi huo, kwa
kuwa sina tatizo lolote na Ndugu
Kibanda na wala nisingependa
lililomtokea limtokee yeye wala mtu
mwingine yeyote.
Ni imani yangu ya dhati kwamba
vyombo husika katika nchi yetu
havitasita kulitalifanyia kazi jambo
hili na ukweli juu ya nini
kimemtokea Bwana Absalom
Kibanda utajulikana na kuwekwa
bayana.
Mwisho, shukrani kwa wote
mlionipigia simu kuhusu hili, tuko
pamoja na nawatakia kila la kheri
katika shughuli za ujenzi wa Taifa
letu hili la Tanzania ambalo msingi
wake umejengwa katika haki, umoja,
amani na kujali hali za watu wake.
Asanteni sana.
Ndugu yenu,
Ridhiwani Kikwete,
Dar es Salaam, Jumapili Machi 17,
2013.