Header Ads

test

Alichokisema ZITTO KABWE baada ya mlipuko


Februari 20, 2013 niliandika kwenye
gazeti la RaiaMwema suala fulani,
kufuatia matukio ya kulaaniwa ya
#Arusha Leo. Pia kufuatia mijadala
inayoendelea kuhusu #Udini nimeona
vema nirejee sehemu ya Makala ile;
"Viongozi wamekuwa wakitoa kauli za
kugawa wananchi. Kiongozi wa CCM
kwa mfano anaposema CUF ni chama
cha Waislam, anawaambiwa waislam
nendeni huko ndio chama chenu.
Kiongozi wa CCM anaposema
CHADEMA ni chama cha kikristo,
anawaambia wakristo nendeni huko
ndio chama chenu. Mwanachama wa
CHADEMA anapotoa taarifa kuonyesha
kuwa CCM inapendelea waislamu,
anadhihirisha kuwa kweli chama
chake hakipendi waislamu. Viongozi
wa kisiasa wanatoa kauli majukwaani
bila kuzipima na kugawa wananchi.
Baadhi ya taasisi za kidini zimekuwa
zikutumiwa na vyama vya siasa
kusambaza chuki hizi kwenye jamii.
Mimi ni Mtanzania. Taifa ambalo
limejengwa kwenye misingi ya usawa
na haki. Misingi ya Umoja na
mshikamano. Tunu zetu ni hizo na
sio dini zetu. Viongozi
wanapoendelea kulea upuuzi huu wa
udini Taifa litapasuka vipande
vipande. Kwenye masuala ya udini
watu hawaweki akili, wanaongozwa na
imani. Mijadala inayoendelea sasa
inatugawa sana. Lazima tukatae.
Tuseme udini sio tunu ya Taifa letu,
inaweza kuwa tunu ya mtu binafsi
lakini Utanzania wangu ni utu, umoja,
uzalendo, uwajibikaji na uadilifu.
Mtu yeyote yule anayepanda mbegu
za udini asionewe aibu.
Ashughulikiwe haraka sana. Wapuuzi
Fulani wanasema kwa kuwa Mkuu wa
Polisi ni wa dini Fulani basi ndio
maana hachukui hatua. Huyu sio
Mkuu wa polisi wa kwanza nchini wa
dini hiyo, kuna aliyekuwepo na
akaingiza msikitini askari polisi na
viatu. Tusiruhusu kabisa upuuzi huu
kwamba watu wenye dini Fulani
hawachukui hatua dhidi ya watu wa
dini zao. Vyombo vya usalama vijue,
mtu anayeua ni muuaji tuna lazima
achukuliwe hatua kwa uuaji wake.
Tena uuaji mbaya unaojenga chuki
kwa nchi yetu. Mtu anayetamka
maneno ya chuki dhidi ya dini
nyingine achukuliwe hatua bila kujali
hadhi yake.
Mwisho hatuna namna, ni lazima
Taifa liongee. Lazima tuwe na
mjadala wa wazi na wa kuheshimiana
kuhusu masuala ya udini na
kuvumiliana kidini. Hatuwezi kuweka
rehani amani ya nchi yetu kwa suala
la kuswali au kusali. Badala ya
kurushiana lawama, tuzungumze kwa
uwazi. Makundi ya wananchi wenye
kuona uonevu wa kidini waje waseme
kwa uwazi na masuala hayo kujadiliwa
kwa uwazi. Muhimu tupate mwafaka
na kujenga Taifa imara na lenye
mshikamano.
Kwa nchi yenye utajiri wa rasilimali
kama yetu udini ni kichocheo tosha
cha vita ya wenyewe kwa wenyewe na
migogoro isiyokwisha. Ni lazima
tuchukue hatua sasa.
Tuache unafiki wa kunyoosheana
kidole. Kila mtu atazame nafsi yake
na aseme ukweli wake kwa uwazi
kabisa. Tusifukie uchafu chini ya
kapeti.