WATUHUMIWA WA MLIPUKO WA BOMU OLASITI WAACHIWA HURU
POLISI Jijini Arusha imewaachia kwa
dhamana watu wanaotuhumiwa kurusha bomu kwenye Kanisa la Mtakatifu
Joseph Mfanyakazi, Olasiti, lililopo Jijini hapa. Aidha Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema, wanaendelea kuwahoji
zaidi watu hao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo,
Kamanda Sabas amesema, wameamua kuwaachia kwa sababu sheria haiwaruhusu
kuendelea kuwashikilia muda mrefu.
“Na lengo letu hasa katika hili tukio hatutaki kumwonea mtu yeyote, ndio sababu tunafanya uchunguzi wa kina,” alisema Sabas.
Alisema watuhumiwa hao ni lazima
waripoti polisi, pale wanapohitajika. Alisema hadi sasa hakuna mtu
mwingine aliyekamatwa au kufikishwa mahakamani zaidi ya Victor Ambros
aliyefikishwa mahakamani.
Ambros alifikishwa mahakamani na
kusomewa mashitaka ya kuua na kukusudia kuua huku wengine wanne, raia wa
nje ya nchi wakiachiwa huru.
Awali watuhumiwa waliokuwa wakiendelea
kushikiliwa kwa uchunguzi zaidi ni Jassini Mbarak (29) mkazi wa Bondeni
Arusha, Joseph Lomayani (18) dereva wa pikipiki mkazi wa Kwa Mrombo
Arusha, Batholomeo Silayo (23) mfanyabiashara mkazi wa Olasiti na
Mohamed Suleiman Said (38) mkazi wa Ilala Jijini Dar es Salaam.
Raia wa Falme za Kiarabu ambao wote
walioachiwa huru, ni Abdulaziz Mubarak (30) (Saudi Arabia), Foud Saleem
Ahmed (28), Said Mohsen na Said Abdallah Said (28).
Wote wanaishi nchini humo. Bomu hilo
lililorushwa Mei 5, mwaka huu, saa 4.30 asubuhi, lilisababisha vifo vya
watu watatu na majeruhi wapatao 60.
Majeruhi hao walipatiwa matibabu katika
Hospitali za Mount Meru na St. Elizabeth na baadhi yao walihamishiwa
Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Katika ibada hiyo ya uzinduzi wa Parokia
mpya ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, mgeni rasmi alikuwa Balozi wa
Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisco Padilla, akisaidiana na Askofu wa
Jimbo Kuu la Arusha, Joseph Lebulu.
source by HABARILEO
Post a Comment